Ijumaa 23 Oktoba 2026 - 13:30
Mwamko wa Umma wa Kiislamu Utapatikana kwa Kurejea kwenye Nafasi Yake ya Kistaarabu na Ujumbe Wake wa Kimataifa

Hawza/ Dkt. Mansur Mandur, mwanazuoni wa Al-Azhar, amesisitiza kuwa; mwamko wa Umma wa Kiislamu utapatikana kwa kurejea kwenye nafasi yake ya kistaarabu na ujumbe wake wa kimataifa, kupitia kuhuisha mwamko wake, kuimarisha umoja wa Waislamu na kushikamana na mafundisho ya Qur’ani Tukufu.

Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Dkt. Mansur Mandur, mwandishi na mhadhiri wa Kimisri na miongoni mwa wanazuoni wa Al-Azhar, alitoa matamshi hayo katika Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa “Mwamko wa Umma wa Muhammad (s.a.w.w.)”, uliofanyika Jumatano, tarehe 29 Mehr 1405, kwa juhudi za Jumuiya ya Kimataifa ya Qadimun.

Akisisitiza umuhimu wa kufufua ujumbe wa kihistoria wa Umma wa Kiislamu, kuimarisha umoja wa Waislamu na kurejea kwenye mafundisho ya Qur’ani Tukufu, alisema kuwa Umma wa Kiislamu unahitaji kuhuisha mwamko wake, kufanya upya ahadi yake kwa Mwenyezi Mungu na kutambua upya wajibu wake wa kidini na kijamii ili uweze kutekeleza nafasi yake duniani.

Dkt. Mansur Mandur, akizungumzia nafasi ya pekee uliyopewa Umma wa Kiislamu katika Qur’ani Tukufu, alisema kuwa Umma huu ni umma wenye upekee, ambao uhusiano wake na Mwenyezi Mungu umejengwa kupitia wahyi wa Mwenyezi Mungu. Aidha, umepewa mfumo, lengo na katiba iliyo wazi ya kufuata katika safari yake ya maisha, ambayo unapaswa kuirejea katika nyanja zote za maisha ya mtu binafsi na jamii.

Akirejelea aya ya 110 ya Suratul Aal-Imran, inayosema:

كُنْتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنْكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ

“Nyinyi mmekuwa umma bora kabisa uliotolewa kwa ajili ya watu; mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamwamini Mwenyezi Mungu.”

Alieleza kuwa; nafasi ya Umma wa Kiislamu si cheo cha heshima kwa jina tu, bali imeubebesha umma huu jukumu kubwa la kuleta marekebisho duniani, kupambana na dhuluma na ufisadi, na kueneza tunu za Mwenyezi Mungu.

Mwanazuoni huyo wa Kimisri aliongeza kuwa kauli ya Qur’ani “أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ” — “uliotolewa kwa ajili ya watu” — inahitaji kutafakariwa kwa kina, kwa sababu inaonesha kuwa Umma wa Kiislamu unapaswa kuwa na uwezo wa kukabiliana na masuala na matatizo yanayoikabili jamii ya wanadamu kwa kutegemea mwongozo wa Mwenyezi Mungu. Alifafanua kuwa kuamrisha mema na kukataza maovu ni miongoni mwa majukumu muhimu zaidi ya umma huu katika kutekeleza ujumbe wa Mwenyezi Mungu.

Dkt. Mansur Mandur, akirejelea aya ya 122 ya Suratut Tawba kuhusu umuhimu wa kupata ufahamu wa kina wa dini na kuielimisha jamii, alisisitiza kuwa; si lazima kila mwanajamii wa Umma wa Kiislamu awe mwanazuoni wa dini. Badala yake, kunapaswa kuwa na kundi la watu wenye ufahamu wa kina wa dini na wanaoelewa malengo ya mafundisho yake, ambao watatekeleza jukumu la kuelimisha na kuiongoza jamii. Hilo litawawezesha watu kuyatambua kwa usahihi majukumu yao ya kidini na kijamii.

Vilevile, akirejelea aya ya 41 ya Suratul Hajj, alitaja kusimamisha Swala, kutoa Zaka, kuamrisha mema na kukataza maovu kuwa ni miongoni mwa sifa za jamii iliyopata uwezo na kuimarika katika ardhi. Alisema kuwa, kwa mujibu wa mtazamo wa Qur’ani, nguvu na uwezo wa kujitegemea hupata maana yake pale vinapoambatana na kuwajibika na kutekeleza tunu za Mwenyezi Mungu.

Mhadhiri huyo wa Kimisri, akizungumzia mwenendo wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) katika kufundisha namna ya kufanya ijitihadi na kutoa hukumu, alisisitiza umuhimu wa kurejea kwenye vyanzo halisi vya Uislamu. Aliongeza kuwa katika kufanya maamuzi na kutoa hukumu, Umma wa Kiislamu unapaswa kuzingatia misingi ya uadilifu, mafundisho ya Qur’ani na Sunna za Mtume (s.a.w.w.), huku ukijiepusha na ubaguzi, upendeleo usio sahihi na kufuata matamanio ya nafsi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha